Highlights

Mfanyabiashara wa mifugo auawa kwa risasi Merille

Na Caroline Waforo

Mfanyabiashara mmoja wa mifugo ameuawa kwa kupigwa risasi alfajiri ya leo Jumanne katika eneo la Merille kaunti ya Marsabit.

Marehemu Elias Irbae mwenye umri wa makamo alipigwa risasi mgongoni baada ya kushuka basi akitokea Nairobi, ambapo alikuwa ameandamana na wenzake watatu kwa shughuli za biashara katika soko la Merille kabla ya kukumbana na kifo chake.

Akithibitisha tukio hilo, Kaimu Kamanda wa polisi Marsabit George Kipkoros amesema kuwa uchunguzi unaendelea ili kubaini kiini cha mauaji hayo.

Kipkoros amebaini kuwa washukiwa hawakuiba chochote baada ya kupatikana kwa kiasi cha shilingi 298,000 alichokuwa nacho marehemu.

Wafanyabishara katika soko hilo la Merille wameitaka idara ya usalama kuhakikisha kuwa wote waliohusika na mauaji ya mfanyabiashara huyo wa kuuza na kununua mbuzi kati ya Nairobi na Marsabit wamekamatwa na kuwajibishwa kisheria.

Kutokana na mauaji hayo wafanyabiashara kutoka soko la Kiamaiko kaunti ya Nairobi wametishia kusitisha biashara na wenzao wa Merille wakieleza hofu ya usalama wao.

Hata hivyo, wafanyabiashara hao wamehakikishiwa usalama wa kutosha huku wakihimizwa kuwa na subira huku uchunguzi ukiendelea.

Kaimu Kamanda Kipkoros ametoa hakikisho kuwa waliotekeleza mauaji hayo watakamatwa na kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria.

Post Comment