IEBC yapinga madai ya kutupilia mbali sajili ya zamani ya wapiga kura
Na Nyabande Orwa
Tume ya IEBC imepinga madai ya kutupilia mbali rejista ya wapiga kura ya kabla ya katiba ya mwaka 2010.
Akizungumza na kituo hiki baada ya kuhudhuria hafla ya kuhamasisha wakazi wa eneo bunge la Saku kujiandikisha kama wapiga kura, kamishna wa IEBC, Alutalala Mukwana, amesema kuwa wanaopaswa kujisajili ni wale walio katika sajili ya zamani ambayo haikuwa ya kidijitali.
Wakati huo huo, amepuuzilia mbali madai ya udanganyifu katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027, akisema kuwa makamishna wa sasa wako mbioni kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki.
Alutalala amesema kuwa zoezi la usajili endelevu linaloendelea na linalotarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu tariki 28, limechangia pakubwa kushughulikia changamoto ya umbali na ukubwa wa kaunti ya Marsabit, huku maafisa wa IEBC wakifanikiwa kufika mashinani.
Wakazi waliohudhuria hafla hiyo iliyofanyika katika eneo la Kalro, wameelezea kuridhishwa na hatua zilizopigwa na IEBC katika kuwafikia wananchi, huku wakihamasisha wengine kujitokeza kwa wingi kujiandikisha ili kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao.
Kwa mujibu wa mkuu wa IEBC kaunti ya Marsabit, Sanchan Lokadio, tume hiyo imefanikiwa kuandikisha takriban wapiga kura 18,000 kufikia sasa, huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka kabla ya zoezi hilo kukamilika.



Post Comment