Highlights

Kaunti ya Marsabit kushuhudia mchanganyiko wa hali ya hewa siku saba zijazo.

Na Samuel Kosgei


Wakazi wa Kaunti ya Marsabit wanatarajiwa kushuhudia mchanganyiko wa hali ya hewa kuanzia leo tarehe 21 hadi 27 Aprili, huku maeneo mengi yakipata vipindi vya mawingu, joto kali na mvua chache mwanzoni mwa wiki.

Kwa mujibu wa utabiri huo, maeneo ya Marsabit Town, Karare na Sagante/Jaldesa eneobunge la Saku yataanza wiki kwa hali ya mawingu kiasi na uwezekano wa mvua nyepesi za hapa na pale kati ya leo tarehe 21 na Aprili 22.

Hata hivyo, mvua hizo zinatarajiwa kupungua kufikia tarehe 23 na 24 Aprili kabla ya hali ya jua na ukavu kutawala kuanzia tarehe 25 hadi 27 Aprili.

Joto litakuwa kati ya nyuzi 26 hadi 30, huku ukungu katika maeneo ya mlima Marsabit ukitarajiwa kupunguza mwonekano barabarani hasa nyakati za asubuhi.

Katika eneo la North Horr likiwemo Dukana, Maikona na Turbi, hali ya joto kali na ukavu inatarajiwa kutawala kwa muda mwingi wa wiki, isipokuwa uwezekano mdogo wa mvua fupi mwanzoni mwa wiki. Joto katika maeneo haya linaweza kufikia kati ya nyuzi 30 hadi 35.

Kwa upande wa Laisamis pamoja na maeneo ya Kargi/South Horr na Loiyangalani, mvua za hapa na pale zinatarajiwa mwanzoni mwa wiki kabla ya hali ya mawingu na jua kuchukua nafasi katikati ya wiki. Mwishoni mwa wiki, hali ya ukavu pamoja na upepo mkali na vumbi huenda vikashuhudiwa.

Katika eneo la Moyale, Sololo, Uran na Golbo, mvua nyepesi hadi za wastani zinatarajiwa mwanzoni mwa wiki, kabla ya kupungua na kuacha hali ya jua na ukavu kuelekea mwishoni mwa wiki. Joto katika eneo hili litakuwa kati ya nyuzi 27 hadi 31.

Kwa ujumla, maeneo ya tambarare kama North Horr, Dukana na Illeret yanatarajiwa kuwa na joto kali la nyuzi 30 hadi 34, huku maeneo ya milimani na mashariki kama Sololo na Moyale yakitarajiwa kuwa na hali ya baridi kiasi ya nyuzi 24 hadi 28 kutokana na mawingu na mvua chache.

Post Comment