Mashaka yatawala baada ya ahadi za ikulu kwa Marsabit
Na Nyabande Orwa
Siku chache baada ya ziara ya viongozi na wakazi wa kaunti ya Marsabit katika Ikulu ya Nairobi, baadhi ya wakazi wa kaunti hii wameonyesha kutoridhishwa na ahadi zilizotolewa na Rais William Ruto wakati wa mkutano huo.
Wakizungumza na kituo hiki, wakazi hao wamesema kuwa ahadi nyingi zilizotolewa na serikali hii wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita bado hazijatekelezwa. Kutokana na hali hiyo, wanasema hawana imani kwamba ahadi mpya zilizotolewa katika mkutano wa Ikulu zitatekelezwa.
Wakazi hao wameeleza kuwa Marsabit bado inakabiliwa na changamoto nyingi za maendeleo ambazo zimeendelea kuwepo kwa muda mrefu bila kupatiwa suluhu la kudumu.
Wakati huo huo, wakazi hao wanadai kuwa ziara hiyo ilikuwa jukwaa la viongozi kujipigia debe kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. Pia wameilalamikia serikali kwa kuchelewesha kushughulikia tatizo la ukosefu wa umeme wa uhakika katika kaunti hii, licha ya Loiyangalani, kuwa miongoni mwa maeneo yanayozalisha nishati ya umeme kwa kutumia upepo.



Post Comment