Highlights

Marsabit yazindua kituo cha mawasiliano ya dharura kuimarisha huduma za ambulensi.

Na Samuel Kosgei

Huduma za dharura za matibabu katika Kaunti ya Marsabit zinatarajiwa kuimarika kufuatia uzinduzi wa kituo cha mawasiliano ya dharura kitakachoratibu mwitikio wa ambulensi pindi ajali au tukio la dharura linapotokea katika maeneo mbalimbali ya kaunti.

Kituo hicho kimeanzishwa kupitia ushirikiano kati ya Serikali ya Kaunti ya Marsabit na mashirika yasiyo ya kiserikali, huku pia sera za kuongoza utoaji wa huduma za dharura zikizinduliwa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Naibu Gavana wa Marsabit, Solomon Gubo, alisema kituo hicho kitasaidia kuimarisha uratibu wa huduma za dharura na kuhakikisha ambulensi zinafika kwa haraka katika maeneo yanayohitaji msaada.

“Kupitia kituo hiki cha mawasiliano, tutakuwa na uwezo wa kupokea taarifa za dharura kwa wakati na kuelekeza ambulensi katika eneo husika kwa haraka zaidi. Hii ni hatua muhimu katika kuokoa maisha ya wananchi,” alisema Gubo.

Aliongeza kuwa serikali ya kaunti imeweka sera zitakazoboresha utoaji wa huduma za dharura na kuhakikisha huduma hizo zinatolewa kwa viwango vinavyokubalika.

Gubo pia aliwataka wauguzi na wafanyakazi wa sekta ya afya kuendelea kuhudumia wananchi kwa kujitolea licha ya changamoto zinazokabili sekta hiyo.

“Nawapongeza wafanyakazi wetu wa afya kwa kujitolea kwao licha ya changamoto zinazotokana na ukubwa wa kaunti na mazingira magumu ya kufikisha huduma kwa wananchi,” alisema.

Kwa upande wake, mwakilishi wa shirika la Ambulensi, Bethwell Aliwa, alisema shirika hilo tayari limeweka mitambo saba ya kufuatilia magari ya ambulensi katika maeneo mbalimbali ya Marsabit ili kuboresha mwitikio wa huduma za dharura. Japo kuna magari ya ambulensi 19 Marsabit nyingi anasema haziko katika hali sawa.

“Hapo awali hakukuwa na mfumo madhubuti wa kuratibu huduma za dharura katika kaunti. Kupitia ushirikiano huu, tumeanzisha mfumo utakaowezesha mwitikio wa haraka na hivyo kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika,” alisema Aliwa.

Naye Meneja wa Programu wa Malteser International, Robert Pampula, alisema pamoja na mafanikio yaliyopatikana, bado kuna changamoto zinazohitaji kushughulikiwa ili kuboresha huduma za dharura.

“Ukubwa wa Kaunti ya Marsabit, hali mbaya ya barabara na idadi ndogo ya magari ya ambulensi bado vinazuia utoaji wa huduma za dharura kwa ufanisi. Hata hivyo, tunaendelea kushirikiana na serikali na wadau wengine kuboresha mfumo huu,” alisema Pampula.

Wadau waliohudhuria uzinduzi huo walieleza matumaini kuwa mfumo mpya wa mawasiliano ya dharura utachangia kupunguza muda wa mwitikio wa ambulensi na kuongeza nafasi ya kuokoa maisha ya waathiriwa wa ajali na wagonjwa wanaohitaji huduma za dharura katika maeneo mbalimbali ya Kaunti ya Marsabit.

Post Comment