Loading Now

Highlights

Mahakama ya Marsabit yaadhimisha siku ya mazungumzo na raia

NA Samuel Kosgei

Afisa wa masuala ya watoto katika Kaunti ya Marsabit, Leakey Mukanzi, ametoa wito kwa washikadau kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana na visa vya dhulma za kijinsia dhidi ya watoto wa kike.

Akizungumza wakati wa kikao cha siku ya mazungumzo kati ya mahakama na wananchi, kilichowaleta pamoja wanajamii, mashirika ya kijamii na maafisa wa idara ya mahakama, Mukanzi amesema kuwa ofisi yake tayari imepokea visa vinne vya unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto wa kike, idadi ambayo amesema ni kubwa na ya kutia wasiwasi.

Aidha, Mukanzi ameitaka jamii kuripoti mara moja visa vya unyanyasaji wa kingono ili kulinda na kuokoa maisha ya mtoto wa kike.

Wakati huo huo, Mkurugenzi wa shirika la Marsabit Women Advocacy Development Organization (MWADO), Nuria Gollo, amewataka wazazi kuanza kuwapa watoto wa kike elimu mapema kuhusu watu wanaofaa kuhusiana nao kama njia mojawapo ya kuzuia visa vya dhulma za kijinsia.

Akizungumzia ongezeko la visa vya watoto wa kike kuavya mimba Marsabit, Gollo amesuta vikali wahusika na kutoa wito kwa idara ya mahakama kukaza kamba ili kuhakikisha kuwa washukiwa wanachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria.

Post Comment