Highlights

Idara ya maji Marsabit yasema inashughulikia malalamishi ya wakaazi wa Bori

NA Caroline Waforo

Baada ya wakaazi wa eneo la Bori eneobunge la Moyale kaunti ya Marsabit kushiriki maandamano kulalamikia ukosefu wa maji na huduma nyingine muhimu, idara ya maji jimboni imesema kuwa iko mbioni kuweka mikakati ya kutatua tatizo hilo.

Akizungumza na wanahabari leo Jumatano, Mkurugenzi wa huduma za maji katika kaunti ya Marsabit Umuro Sharamo amesema kuwa idara hiyo ina mpango wa kuchimba kisima kipya katika eneo hilo na pia kukarabati kisima kilichoharibika.

Sharamo amewataka wakaazi hao kuwa na subira huku juhudi za kutafuta suluhu ya kudumu zikiendelea.

Kwa upande wake msemaji wa serikali ya kaunti ya Marsabit Abduba Barille, ameitaka jamii ya Bori na wakaazi kote jimboni kuhahakikisha wanapendekeza miradi ya maji pamoja na miradi mingine muhimu, wakati wa vikao vya ushirikishwaji wa umma ili mahitaji yao yajumuishwe kwenye mipango ya maendeleo.

Mapema wiki hii wakaazi wa Bori waliandamana huku wakishutumu viongozi wao wa mashinani na wa jimbo kwa kuwapuuza na kutowatafutia suluhu la matatizo wanayopitia.

Masuala mengine yaliyoibuliwa na wakaazi hao ni ikiwemo huduma duni za matibabu, barabara mbovu na ukosefu wa mtandao wa simu suala wanalosema linazuia kilio chao kusikika.

Wakaazi walitoa wito kwa rais William Ruto kuingilia kati na kuwanusuru kwani viongozi wao wamewapuuza na kufumbia jicho matatizo yao.

Post Comment