Serikali ya kaunti ya Marsabit yaondolea wazazi wasiwasi kuhusu hatima ya ufadhili wa elimu.
January 21, 2025
Washukiwa wawili wa wizi wa kimabavu wamekamatwa mjini Marsabit.
Wawili hao Boru Wako almaarufu Wako Abakula na Abdirahman Hussein almaarufu Churuka walikamatwa mwishoni mwa wiki kwa kuhusishwa na visa mbalimbali vya wizi wa kimabavu mjini Marsabit na viunga vyake.
Akithibitisha hili OCPD wa Marsabit Central Edward Ndirangu amesema kuwa wawili hao ni kati ya washukiwa kadhaa wanaowindwa kwa kuhusika na visa hivi.
Mshukiwa wa kwanza Boru Wako ambaye ni mwanachama wa genge la watu sita alikamatwa siku ya Ijumaa iliyopita katika eneo la Harobota huku maafisa wa polisi wakifanikiwa kunasa bodaboda inayoaminika kutumika katika kutekeleza uhalifu.
Boru aliyenaswa na camera fiche za CCTV anahusishwa na visa kadhaa vya wizi wa kimabavu vya hivi maajuzi ikiwemo kisa ambapo kijana moja wa umri wa miaka 18 alijeruhiwa kwa kupigwa risasi tumboni katika kisa cha wizi wa kimabavu katika duka moja mjini Marsabit huku pia wezi wakifanikiwa kuiba kiwango cha fedha kisichojulikana kutoka kwa mhudumu wa duka hilo tarehe 21 mwezi uliopita wa Octoba.
Pia anahusishwa na wizi wa kimabavu katika mtaa wa Nyayo Road usiku wa kuamkia Novemba tarehe 7.
Naye Churuka ambaye ashawahi kutumikia kifungo gerezani kwa kosa la uhalifu alikamatwa siku ya Jumamosi iliyopita kwa kuhusishwa na visa kadhaa ikiwemo wizi wa simu pamoja na uvunjaji wa maduka mjini Marsabit akiwa amejihami kwa silaha butu.
Churuka mwanachama wa genge la watu watatu alikamatwa katika maeneo la Stage 44.
Wawili hao wamefikishwa katika mahakama ya Marsabit leo hii mbele ya hakimu mkuu mwanadamizi Christine Wekesa ambapo upande wa mashtaka umeomba siku 7 kuwazuiliwa washukiwa hao ili kuendeleza uchunguzi.
OCPD Ndirangu amewataka wakaazi jimboni kushirikiana na idara ya usalama kwa kutoa taarifa muhimu ili kukomesha magenge haya yanayoendelea kuwahangaisha wananchi.