Idadi chache ya wanafunzi waripoti shuleni wiki ya kwanza ya muhula huu…
January 10, 2025
Wazazi wa wanafunzi 131 wa shule ya upili ya Goro Rukesa watakiwa kuwa na subira, uchunguzi unapoendelea.
Wazazi wa wanafunzi 131 wa shule ya upili ya Goro Rukesa iliyoko eneo bunge la Saku kaunti ya Marsabit, ambao matokeo ya mitihani yao ya KCSE imeshikiliwa na baraza la mitihani nchini KNEC wametakiwa kuwa na subira wakati baraza hilo linapoendeleza uchunguzi wake.
Kwa mujibu wa mkurugenzi wa elimu katika kaunti ya Marsabit Peter Magiri ni kuwa uamuzi kuhusiana na matokeo ya wanafunzi hao utafanywa na baraza la mitihani KNEC baada ya uchunguzi wa kubaini iwapo walishiriki katika zoezi la udanganyifu wa mitihani au la kukamilika.
Akizungumza na shajara ya Radio Jangwani ofisini mwake, Magiri amekariri kuwa KNEC itafuata mikakati yote iliyowekwa na hivyo hakuna hoja ya wazazi kuwa na wasiwasi wowote.
Amesema kuwa kufikia sasa matokeo ya shule ya upili ya wasichana ya Bishop Cavalera yanaashiria kwamba ndio shule iliyofanya vyema zaidi jimboni huku wanafunzi 53 kati 54 waliokalia mtihani wa KCSE 2024 wakipata alama ya C Plus kwenda juu.
Aidha Magiri ametaja kufurahishwa na matokeo ya baadhi ya shule ambazo zinakua huku akizidi kuzimotoisha kutia bidii.
Mkuu huyo wa elimu jimboni Marsabit amepongeza baadhi ya shule kutokana na matokeo bora ambayo ameyataja kwamba yametokana na kujitolea kwa walimu, wazazi na hata wanafunzi binafsi.