Wazazi wa shule ya upili ya Sasura girls wamkataa mwalimu mkuu mpya aliyehamishiwa shuleni humo.
January 14, 2025
Wazazi wa shule ya upili ya Sasura girls iliyo eneo la Qubi Bagasa eneo bunge la Saku kaunti ya Marsabit wamejitokeza na kupinga hatua ya tume ya kuajiri walimu nchini TSC kubadilisha uongozi wa shule hiyo.
Wazazi hawa wameelezea kutofurahishwa kwao na maamuzi ya kumhamisha hadi shule hiyo Madina Marme ambaye alikuwa mwalimu mkuu wa shule ya upili ya Maikona girls wakisema kuwa hawakuridhishwa na jinsi ambavyo mwalimu huyu alikuwa akiendesha shule hiyo na kuitaka idara ya elimu jimboni kutoa maelezo zaidi kuhusiana na zoezi hilo.
Wakizungumza na meza ya habari ya radio Jangwani wazazi hao wamesema kuwa wangetaka wazazi pamoja na walimu kuhusishwa wakati ambapo maamuzi ya usimamizi wa shule hiyo yanajadiliwa huku wakiwarai viongozi kutoingiza siasa katika masuala ya elimu kwani huenda hilo likalemaza masomo jimboni.
Kwa upande wake Mhubiri Godana Male kutoka kanisa la AIC Dirib Gombo na ambaye amezungumza kwa niaba ya bodi ya shule hiyo amesema kuwa hawakuhusishwa kwa vyovyote vile katika kufanya maamuzi ya kuhamisha mwalimu huyo jambo ambalo liliwakera na kupelekea wao kuandikia TSC barua wakitaka uamuzi huo ubadilishwe.
Aidha mhubiri Godana amesema kuwa ni sharti tume ya kuajiri walimu iwahushe wazazi, bodi ya shule nahata washikadau wengine katika kufanya maamuzi kuhusu uongozi wa shule hiyo.