Wasichana na wanawake Marsabit watakiwa kufanya kozi ya sayansi ili kuendana soko la ajira.
February 11, 2025
Na Samuel Kosgei
Huku ulimwengu leo ikiadhimisha siku ya kimataifa ya wanawake na wasichana katika sayansi wazazi kaunti ya Marsabit wametakiwa kuwatia moyo wasichana wao kufanya kozi zinazohusiana na masomo ya sayansi na hisabati ili kuendana na mahitaji ya ajira.
Afisa mkuu katika idara ya Utamaduni na Jinsia kaunti ya Marsabit Bi Annamaria Denge amesema kuwa wazazi wanafaa kuwatia shime na moyo wasichana wao kutafakari haja ya kutia bidii katika masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hesabu (STEM) ili kuongeza ushindani miongoni mwa wasomi.
Akizungumza nasi ofsini mwake Annamaria amesema kuwa dhana ya jadi kuwa wasichana hawafai kusomea kozi zinazodhaniwa ni ya wavulana ilishapitwa na wakati.
Vile vile amesema kuwa katika kaunti ya Marsabit wanawake na wasichana wengi wameruka kizingiti hicho na wamefanya kozi za sayansi ambazo hufikiriwa kuwa za wavulana. Amewarai wanafunzi kuzingatia soko la ajira miaka ijayo ili kujizatiti masomoni.
Kauli yake hiyo imetiliwa mkazo na Asha Bonaya ambaye ni mtetezi wa jinsia ya kike anayesema kuwa siku hii inatoa hamasisho kwa kuwapa fursa na kuwatia moyo wasichana Marsabit na hata kote ulimwenguni kupambania nafasi zao katika ulingo wa masomo ya sayansi.
Aidha ameambia shajara kuwa na kuwahusisha wanawake katika idara ya sayansi mapema itaimarisha ukuaji wa uchumi na maendeleo siku za mbeleni. Amewarai wasichana kuiga wanawake waliofaulu katika tasnia zao zinazohusu sayansi na hisabati.