Local Bulletins

Mtu mmoja afariki kutokana na ugonjwa wa Kalazaar Marsabit, sita wakipokea matibabu kulingana na serikali ya kaunti.

Na Samuel Kosgei

Mtu mmoja ameripotiwa kuaga dunia kufikia sasa kutokana na ugonjwa wa Kalaazar ambao umetajwa kuwa kero katika maeneo ya Loglogo na Laisamis.

Msemaji wa serikali ya kaunti ya Marsabit Abdub Barile akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa amesema kuwa mwanamke mmoja kutoka eneobunge la Laisamis alifariki akipokea matibabu katika hospitali ya rufaa ya Marsabit wiki hii.

Barille ameongeza kuwa kuanzia mwezi January hadi mwezi huu wa pili, visa 25 vya Kalazaar vimerekodiwa na idara ya afya ya umma jimboni suala alilosema linatia hofu na wasiwasi kwani katika miaka ya nyuma visa havikupanda kwa kasi hiyo.

Kufikia sasa anasema kuwa wagonjwa sita wanapokea matibabu hospitalini na wanapokea matibabu katika hospitali za umma ikiwemo laisamis ambayo ina mgonjwa mmoja, Moyale wagonjwa wawili na hospitali ya rufaa ya Marsabit ina wagonjwa 3.

Serikali ya kaunti kupitia idara ya afya anasema imeweka mikakati ili kudhibiti hali hiyo ambayo imekuwa tishio kwa umma. Anasema kuwa dawa tayari imewasilishwa katika hospitali husika na wanalenga kunyunyizia dawa maeneo athirika kuanzia wiki ijayo

Subscribe to eNewsletter