Wakazi wa vijiji vya Nawapa,Kulamawe na Kilimambogo Loiyangalani,wamelalamikia uhaba wa maji…
January 15, 2025
Idara ya kitaifa ya kutathmini takwimu (KNBS) kwenye ripoti yake ya hivi punde imesema kuwa kaunti ya Marsabit ni mojawapo ya kaunti zinazokua kimaendeleo kwa kasi nchini miaka ya hivi karibuni.
Kwenye ripoti yake hapo jana shirika hilo la takwimu limesema kuwa Marsabit imekua kiuchumi kwa asilimia 9.3 ikiongoza orodha ya kaunti kaunti 10 zinazofanya vyema kuanzia mwaka wa 2019 – 2023.
Kaunti nyingine zilizofanya vyema kwa kipindi hicho cha miaka 5 ni pamoja na Nairobi na Nakuru ambayo ilipata alama za kuvutia na kuimarisha nafasi zao kama vivutio vya uwekezaji.
Japo changamoto kuu imetajwa kuwa ukosefu wa usalama wakati mwingine, Kaunti ya Marsabit inatajwa kukua kutokana na kuongezeka kwa shughuli katika sekta za maji na sekta ya ujenzi kulingana na ripoti ya hivi karibuni ya Mapato ya Jumla ya Kaunti (GCP), ambayo hupima jinsi utajiri unasambazwa miongoni mwa vitengo 47 vilivyogatuliwa.
Baadhi ya wakaazi wa Marsabit waliosema na Radio Jangwani wametoa maoni kinzani baadhi yao wakisema kuwa wameona mabadiliko kadhaa ikilinganishwa na miaka ya nyuma japo wengine pia wamekana kuona maendeleo yoyote kaunti ya Marsabit. Hizi hapa baadhi ya maoni ya wakaazi.
Kaunti nyingine zilizotajwa kufanya vyema ni pamoja na Tana River, Kajiado, Nairobi City, Isiolo, Lamu, Samburu, Turkana na Uasin Gishu.
Zinazojivuta kwenye ukuaji ni pamoja na Embu, Elgeyo Marakwet, Nyamira, Bungoma, Kisii, Garissa na Migori.