Local Bulletins

Baadhi ya magavana wapinga mfumo mpya wa ugavi wa fedha kwa serikali za kaunti unaopendekezwa na Tume ya Ugavi wa Mapato kwa kaunti, CRA.

Baadhi ya Magavana, yule wa  Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir na Julius Malombe wa Kitui wamepinga mfumo mpya wa ugavi wa fedha kwa serikali za kaunti unaopendekezwa na Tume ya Ugavi wa Mapato kwa kaunti, CRA.
Mfumo huo mpya uliopendekezwa na CRA unapendekeza mgao wa shilingi bilioni 417 kwa Kila kaunti huku kaunti zenye idadi kubwa ya watu zikipendekezwa kupokea mgao mkubwa wa fedha.

Magavana hao wameyakosoa mapendekezo ya mfumo huo mpya wa ugavi wa mapato walioutaja kuwa mbaya na haufai wakisema mfumo huo utalemaza maendeleo ya ugatuzi katika baadhi ya kaunti nchini, hasa kutokana na suala la idadi ya watu na vigezo vya umasikini.

Wamesema kuwa kigezo cha idadi ya watu na raslimali au taasisi haipaswi kutumika kwa kuwa wanaoingia katika kaunti hizo na kutumia raslimali kama vile hospitali ni wengi ikilinganishwa na takwimu za idadi ya watu iliyofanyika wakati wa usiku.

Haya yanajiri huku ikibainika kuwa huenda zaidi ya kaunti 20 zikaathirika kwa kupata mgao mdogo wa mapato ukilinganisha na mgao wa hapo awali iwapo mfumo mpya huo unaopendekezwa na Tume ya Ugavi wa Mapato, CRA utaidhinishwa na Bunge.

Katika mapendekezo hayo ya mfumo mpya wa ugavi wa mapato, Mkuu wa CRA, Mary Chebukati amesema kaunti zenye idadi kubwa ya watu zitapokea mgao zaidi huku idadi ya watu ikikadiriwa kuwa asilimia 42 kutoka asilimia 18 katika mfumo wa sasa.

Katika msingi wa tatu, mfumo uliopitishwa mwaka 2020 wa ugavi wa mapato uliweka ugavi kwa kukadiria idadi ya watu kuwa asilimia 18 na sasa imependekezwa kuongezeka hadi asilimia 42, Sehemu sawa ya mgao kwa sasa ni asilimia 20 ambayo imependekezwa kupanda hadi asilimia 22.

Licha ya kwamba kigezo cha asilimia 42 ya idadi ya watu kinaegemea kaunti zenye idadi kubwa ya watu baadhi ya kaunti zilizo na idadi ndogo ya watu zitanufaika na mgao zaidi kutokana na vigezo vya viwango vya umaskini na kiwango cha ukubwa wa ardhi.

Mfumo huo mpya sasa utapunguza mapato kwa kaunti 31, huku kaunti ya Kitui ikitarajiwa kupoteza shilingi milioni 343, nayo kaunti ya Narok ikipoteza shilingi milioni 310 katika mgao ujao.

Mapendekezo hayo tayari yametumwa katika Bunge la Seneti ilinkuzingatiwa huku baraza la magavana likitarajiwa kukutana kutathmini na kuchukua msimamo kuhusu mfumo huo mpya wa ugavi.Ikumbukwe kuwa kikatiba Mfumo wa kubadilisha mgao wa fedha na Tume ya Ugavi wa Mapato CRA, kwa serikali za kaunti hufanywa kila baada ya miaka 5.

Subscribe to eNewsletter