WAZAZI WAMETAKIWA KUWALINDA WANAO MSIMU HUU WA MVUA ZA VULI
November 28, 2024
Baadhi ya Machifu kaunti ya Marsabit, wamewataka wazazi kuwa makini na watoto wao.
Katika wito wao, machifu wameeleza umuhimu wa kuhakikisha usalama wa watoto, hususan wakati huu wa mvua.
Wamesisitiza kwamba wazazi wasiwaruhusu watoto kuchunga mifugo katika maeneo hatari, kwani hali ya mvua inaweza kuleta mafuriko na hatari nyingine.
Aidha, wazazi wametakiwa kuwa makini na watoto wasicheze karibu na mito, ambapo kuna uwezekano wa kutokea ajali kutokana na mabadiliko ya kiwango cha maji.
Kulingana na machifu hao,ni wajibu wa kila mzazi kulinda watoto wao na kuwapa mwongozo wa kutosha ili kuepuka hatari.
Chifu wa Kurkum, Lora Ndubaiya, amesisitiza umuhimu wa michezo kwa vijana katika eneo lake.
Kulingana na chifu huyo, vijana wamepanga michezo mbalimbali katika juhudi za kuwashughulisha watoto wakati huu wa likizo, michezo ambayo itadumu hadi wiki ya mwisho wa likizo.
Aidha,Chifu Ndubaiya amewataka wazazi kuwapa ruhusa watoto wao kuhudhuria michezo hiyo ili kuwazuia kufanya mambo yasiyofaa.
Kulingana na chifu huyo, michezo itatoa fursa nzuri kwa watoto kujiendeleza na kujenga uhusiano mzuri kati yao.