Local Bulletins

VISA VYA UGONJWA WA SURUA AU MEASLES VYAONGEZEKA HADI 11 KATIKA KAUNTI HII YA MARSABIT.

Na Caroline Waforo

Visa vya ugonjwa wa Surua au measles vimethibitishwa kuongeza kutoka 7 hadi 11 katika kaunti hii ya Marsabit.

Akizungumza na shajara ya radio jangwani kwa njia ya kipekee afisa anayefuatilia magonjwa jimboni Marsabit Qabale Duba amesema kuwa visa hivyo vimerekodiwa katika maeneo bunge ya Moyale na North Horr.

Amedokeza kuwa sampuli 30 zilikusanywa na kufanyiwa uchungzi katika maabara ya kitaifa.

Kulingana na Qabale katika sampuli zilizokusanywa, idadi kubwa ni ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.

Aidha amethibitisha kuwepo kwa maafisa wa nyanjani wanaofuatilia ugonjwa huo kwa karibu.

Qabale pia amedokeza kuwa mlipuko wa ugonjwa huo jimboni unachangiwa pakubwa na mpaka wa Kenya na Ethiopia ambapo watu wanatangamana sana.

Wazazi jimboni Marsabit wametakiwa kuhakikisha kuwa wanao wanapata chanjo dhidi ya ugonjwa huo wa surua.

Ugonjwa wa surua huenea kwa urahisi wakati mtu aliyeambukizwa anapumua, kukohoa, au kupiga chafya nje ya hewa iliyoambukizwa ambayo inapumuliwa na mtu mwenye afya.

Surua pia inaweza kuenea kwa kugusana nyuso au vitu vilivyochafuliwa.

Mara baada ya kuambukizwa, surua inaweza kusababisha ugonjwa mbaya, matatizo mengine na hata kifo.

Surua inaweza kuathiri mtu yeyote, lakini mara nyingi huwaathiri watoto. Kupata chanjo ya surua ndiyo njia bora zaidi ya kuzuia maambukizi ya surua na kuenea kwake.

Wiki iliyopita wizara ya afya inayoongozwa na Waziri Malicha Boru ilikuwa imethibitisha visa 7 pekee.

Subscribe to eNewsletter