Local Bulletins

VIONGOZI WA KIDINI MARSABIT WAWATAKA WAZAZI KULEA WANAO KWA NJIA YA MAADILI

NA JOHN BOSCO NATELENG

Mwenyekiti wa muungano wa viongozi wa Kiislamu kaunti ya Marsabit (MAMLEF) Sheikh Ibrahim Oshe amewataka wazazi katika kaunti ya Marsabit kuchukua majukumu ya kuhakikisha kuwa wamewalea wanawao katika mazingira mema ili kusaidia katika kukabiliana na matumizi ya mihadarati.

Oshe amesema kuwa utepetevu wa ulezi ndio unachangia katika kuongezeka kwa matumizi ya mihadarati jimboni hivo kuwataka wazazi kuwa karibu na wanawao zaidi.

Kiongozi huyu wa dini ameelezea kuwa utepetevu huu umeweza kuchangia pia vijana wengi kukosa kumakinika shuleni hivo kuwafanya wengi kuacha shule na kujitosa kwa makundi mabaya ambayo yanawafunza kutumia mihadarati.

Hata hivyo sheikh Oshe amesema kuwa kando na vijana kutumia mihadarati pia wazee siku hizi wanatumia miraa ambayo inawafanya kuachia wamama majukumu yote ya familia jambo ambalo linapelekea familia nyingi kuzozana.

Kadhalika Sheikh Oshe ametoa wito kwa wazee wa jamii wote jimboni, viongozi wa kidini pamoja na serikali kuungana na kuangazia upya mbinu mbadala ya kuwakwamua vijana katika matumizi ya dawa za kulevya kwani mbinu za hapo awali inaonekana kukosa kuzaa matunda.

 

Subscribe to eNewsletter