Local Bulletins

SERIKALI YATENGEA SHILINGI BILIONI 1 FIDIA KWA WAFUGAJI WALIOATHIRIKA NA KIANGAZI

NA CAROLINE WAFORO

Kaunti za Maeneo Kame nchini Kenya zimepokea msaada mkubwa kutoka kwa Serikali Kuu, ambapo Shilingi Bilioni 1 zimetengwa kama fidia kwa wafugaji waliopoteza mifugo yao kutokana na janga la kiangazi.

Haya yamethibitishwa na Katibu wa Idara ya Maeneo Kame na Nusu Kame (ASALs), Bw. Kello Harsama, ambaye alizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Mpango wa Kati wa Nne (MTP-IV) wa Kaunti ya Marsabit, iliyofanyika jana katika ukumbi wa Kanisa Katoliki.

Bw. Harsama ameeleza kuwa fedha hizi zitasaidia kulipa fidia kwa wafugaji katika jumla ya Kaunti 23 za Maeneo Kame nchini, ambazo zimekumbwa vikali na janga la ukame na kupoteza mifugo yao.

Sambamba na hilo, Serikali imetengea Kaunti ya Marsabit Shilingi Milioni 800 kwa ajili ya miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Aidha, Serikali imetenga Shilingi Milioni 250 katika bajeti ya mwaka 2024 kwa ajili ya kuimarisha biashara ya ngozi ya ng’ombe na mbuzi, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya uhifadhi wa ngozi.

Katika mpango huo wa maendeleo kwa miaka mitano ijayo, Serikali imeahidi kuimarisha pia Mpango wa Hifadhi ya Chakula (Hunger Safety Net) na kusasisha hospitali ya Kaunti ya Marsabit hadi kiwango cha tatu (Level 3).

Haya yote ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Kitaifa na Kaunti za Maeneo Kame kushughulikia changamoto za kiuchumi na kijamii zinazowakabili wananchi wa maeneo hayo.

Subscribe to eNewsletter