Local Bulletins

MARSABIT KUONGOZA JUHUDI ZA USAFI WA MAZINGIRA KATIKA SIKU YA DUNIA YA MAZINGIRA

BY CAROL WAFORO

Wakati ulimwengu umejipanga kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Dunia ya Mazingira, Mamlaka ya Kitaifa ya Mazingira (NEMA) nchini Kenya inapania kuongoza juhudi za usafi katika mji wa Marsabit, kwa ushirikiano na Idara ya Misitu Marsabit (KFS) pamoja na serikali ya kaunti ya Marsabit.

Kadiro Oche, Naibu Msimamizi wa Misitu Marsabit, amezungumzia mipango hii katika mahojiano na idhaa. Oche amesema kuwa shughuli hiyo itahusisha usafi wa mji mzima, na itazingatia madhumuni ya Siku ya Dunia ya Mazingira chini ya kauli mbiu “Ukarabati wa Ardhi, Kuzuia Ukame na Kujenga Uimara dhidi ya Ukame”.

Katika juhudi za kutekeleza azma ya serikali kuu ya kupanda miche bilioni 15 ifikapo 2030, Oche amebainisha kuwa katika shughuli ya kesho, watakapanda zaidi ya miche 2,000. Hii ni sehemu ya lengo la kaunti ya Marsabit la kupanda miti bilioni 2.4 ifikapo mwaka 2030.

Juhudi hizi za usafi na upandaji miti zinalenga kuboresha hali ya mazingira katika eneo la Marsabit, ambalo kimsingi lina changamoto ya uhaba wa rasilimali na ukame. Kwa kufanya hivi, NEMA, KFS na serikali ya kaunti ya Marsabit wanatarajia kuwezesha jamii za Marsabit kuwa na uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kulinda rasilimali za asili.

Maadhimisho ya Siku ya Dunia ya Mazingira yanaonyesha umuhimu wa ushirikiano baina ya taasisi za serikali, jamii na wadau wengine katika kulinda na kuboresha mazingira yetu. Juhudi hizi za Marsabit zinaashiria kuwa pamoja tunaweza kushinda changamoto za kimazingira zinazokabili jamii zetu.

Subscribe to eNewsletter