Local Bulletins

IDARA YA WATOTO MOYALE NA DCI INAWAFUATILIA WATOTO WAWILI WALIOTOWEKA MAJUMA KADHAA YALIYOPITA MOYALE NA SOLOLO.

  

Na Caroline Waforo

Idara ya watoto katika eneo bunge la Moyale kaunti ya Marsabit imesema kuwa kwa ushirikiano na idara ya upelelezi DCI inaendelea kuwatafuta watoto wawili walioripotiwa kutoweka kwa njia tatanishi majuma kadhaa yaliyopita katika maeneo ya Moyale na Sololo.

Kulingana na afisa wa watoto katika eneo bunge hilo Abuudo Roba ni kuwa hawajapata taarifa zozote kuhusu msichana wa miaka 13 aliyetoweka katika eneo la Moyale huku yule wa miaka 15 aliyepotea  Sololo akisema kuwa huenda ni kisa cha ndoa ya mapema.

Aidha ameshtumu wakaazi wa Sololo na ambao wanasemekana kuficha taarifa za aliko mtoto huyo.

Amehoji kuwa visa vya watoto kuripotiwa kutoweka huenda ikiwa ni kutokana na ulanguzi wa binadamu, itikadi kali au hata ndoa za mapema huku mpaka wa Kenya na Ethiopia ukichochea baadhi ya visa hivi.

Ametoa hakikisho kwa familia za watoto hao kuwa watafanya kila juhudi kuhakikisha kuwa wanapatikana salama.

Kadhalika ametoa wito kwa wazazi kuwajibika katika malezi ya wanao.

Subscribe to eNewsletter