Local Bulletins

IDARA YA USALAMA LOIYANGALANI YAKANA KUFADHAISHA KESI ZA DHULMA ZA KIJINSIA GBV.

NA ISAAC WAIHENYA

Naibu kamishna katika kaunti ndogo ya Loiyangalani kaunti ya Marsabit Njihia Kiarie amekanusha madai kwamba maafisa wa usalama katika eneo hilo wamekuwa wakizima vita dhidi ya dhulma za kijinsia kwa kuficha baadhi ya kesi.

Akizungumza na Shajara ya Radio Jangwani kwa njia ya simu DCC Kiarie ametaja kwamba uwepo wa kesi nyingi zinazohusiana na dhulma za kijinsia kutoka eneo hilo mahakamani ni dhihirisho tosha kwamba idara ya usalama katika Loiyangalani haijakuwa ikiwasaza wanaotekeleza uovu huo.

DCC Kiarie amewataka wote walio na lalama kuhusiana na kesi za dhulma za kijinsia ambazo wanahisi kuwa zinalemazwa maafisa wa polisi kufika ofisi mwake ili kupata suluhu.

Vilevile ametoa onyo kwa wote wanaowadhulumu haswa watoto kigono pamoja na wazee ambao hutatua kesi za dhulma za kijinsia vijijini na kupelekea haki kukosekana, kuwa serekali itawachukulia hatua kali za kisheria.

Kadhalika mkuu huyo wa usalama katika eneo la Loiyangalani amewaonya wanaoendeleza kasumba ya wizi wa mifugo pia kuwa chuma chao ki motoni.

 

 

Subscribe to eNewsletter