Local Bulletins

AFISA MMOJA WA DCI AUAWA KATIKA SHAMBULIZI LA KIGAIDI KATIKA ENEO LA LAFEY, KAUNTI YA MANDERA….

Afisa mmoja wa polisi wa kitengo cha idara ya ujasusi DCI ameuawa katika shambulizi la kigaidi katika eneo la Lafey, Kaunti ya Mandera.

Magaidi hao wanaoaminika kuwa wanamgambo wa kundi haramu la Alshabaab walitekeleka shambulizi hilo mapema leo Jumatatu na kutoweka na gari mmoja la polisi.

Mhudumu moja wa kituo kimoja cha mafuta, Mandera na aliyekuwa kwenye gari hilo alipatikana kichakani akiwa na majeraha mabaya na kupelekwa katika hospitali ya rufaa ya Lafey ambapo yuko katika hali mahututi.

Kadhalika wakaazi kadhaa wanaoishi karibu na kituo cha polisi cha lafey wanauguza majeraha ya risasi kufuatia shambulizi hilo.

Maafisa wa Polisi kutoka vitengo mbalimbali walitekeleza operesheni ya kuwasaka magaidi hao bila mafanikio huku ikiaminika kuwa walitorokea nchini jirani.

Ni shambulizi ambalo limekemewa na Mbunge wa Lafey, Mohamed Abdikheir.

Maeneo ya kaskazini mashariki mwa kenya pamoja na Pwani ya Kenya yameathirika na mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa wanamgambo hao.

Ripoti iliyotolewa na Kituo cha Haki za Binadamu na Utafiti wa Sera (CHRIPS) mwezi Juni mwaka huu, ilionyesha kuwa mashambulizi 72 yaliripotiwa katika maeneo ya Kaskazini Mashariki na Pwani mwaka uliopita wa 2023.

Ripoti hiyo ilieleza kuwa Mandera iliongoza kwa mashambulizi ikiripoti mashambulizi 25 ambayo yaliua watu 72, ikifuatiwa na Garissa yenye mashambulizi 23 yaliyosababisha vifo 71.

 

Subscribe to eNewsletter