Local Bulletins

Waziri John Munyes ajiuzulu.

Waziri wa madini na Petroli nchini John Munyes.
Picha;Hisani

Na Isaac Waihenya,

Waziri wa madini na Petroli nchini John Munyes amejiuzulu wadhifa huo ili kujitosa katika siasa.

Munyes ambaye anawania kuwa Gavana wa Kaunti ya Turkana, ametangaza kujiuzulu hii leo kabla ya makataa ya Jumatano,Februari 9 kwa watumishi wa umma wanaowania viti vya kisiasa kujiuzulu nyadhifa zao.

Anakuwa waziri wa pili kwenye Baraza la Mawaziri kujiuzulu baada ya Waziri wa Ugatuzi Charles Keter ambaye alijiuzulu hiyo jana ili kuwania ugavana wa Kaunti ya Kericho.

Mawaziri,makatibu wa utawala pamoja na watumishi wengine  wa Umma wanatarajiwa kujiuzulu nyadhifa zao na kuingia katika ulingo wa kisiasa kati ya hii leo na kesho Jumatano ambayo ndio siku ya mwisho kufanya vile.

Sheria ya Uchaguzi inawataka watumishi wa umma wanaopania kuwania viti vya kisiasa kujiuzulu angalau miezi sita kabla ya tarehe ya Uchaguzi Mkuu.

Viongozi wengine wakuu wa serikali waliojiuzulu ni pamoja na katibu wa utawala katika wizara ya leba Patrick Ntutu, katibu wa utawala katika wizara ya Petroli na Madini John Mosonik, Katibu wa kudumu katika idara ya wanyama pori Fred Segor na katibu wa utawala katika wizara ya Utalii Joseph Boinnet.

 

Subscribe to eNewsletter