Local Bulletins

Mtihani wa darasa la nane KCPE waanza vyema leo kote nchini.

Waziri wa Elimu Profesa George Magoha.
Picha;Hisani

Na Samuel Kosgei,

Mtihani wa darasa la nane (KCPE) umeanza vyema leo kote nchini.

Baraza la Kitaifa la Mitihani nchini KNEC lilisajili jumla ya watahiniwa milioni 1.2 katika vituo 28,316 vya mtihani wa KCPE ikilinganishwa na watahiniwa milioni 1.19 katika vituo 28,467 mwaka wa 2020.

Mwaka huu, jumla ya wanafunzi 831,015 watafanya mtihani huo katika vituo 10,413 kote nchini, ikilinganishwa na wanafunzi 752,981 katika vituo 10,437 waliofanya mtihani huo mwaka wa 2020.

Kulingana na maagizo kutoka kwa Wizara ya Elimu, Naibu Makamishna wa Kaunti (DCC) na Makamishna Wasaidizi wa Kaunti (ACCs) pekee ndio watahusika katika kufungua na kufunga kontena hizo kila siku katika Kaunti Ndogo zao.

Mitihani yote lazima isafirishwe kwa kutumia magari ya serikali na angalau pawepo na afisa mmoja wa polisi.

Wasimamizi wa vituo watafanya kazi na maafisa wa polisi ili kuhakikisha kuwa hakuna karatasi yoyote ya mtihani itakayoonyeshwa kwa mtahiniwa yeyote kabla ya kuanza kwa mitihani wenyewe.

Waziri wa Elimu George Magoha alisimamia zoezi la kusambaza mitihani Siku ya Kwanza ya KCPE 2021 katika Kaunti ya Kakamega.

Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i na Waziri wa ICT Mucheru walisimamia kufunguliwa kwa mitihani ya KCPE  katika miji ya Machakos na Kajiado mtawalia.

Naibu Katibu Wizara ya Mambo ya Ndani, Karanja Kibicho, alisimamia zoezi hilo jijini Nairobi huku katibu Fatuma Chege akisimamia zoezi la usambazaji na kuanza kwa mitihani ya Siku ya Kwanza ya KCPE 2020 katika Kaunti ya Nyeri.

Subscribe to eNewsletter