Local Bulletins

Shughuli Ya Kutafuta Jaji Mkuu Nchini Imeingia Siku Yake Ya Tatu.

Jaji Martha Koome mbele ya tume ya huduma za mahakama JSC.
Picha;Hisani

Na Waihenya Isaac,

Shughuli ya kutafuta jaji mkuu nchini imeingia siku yake ya tatu, huku leo ikiwa ni zamu ya Jaji Martha Koome.

Koome aliyeteuliwa Jaji wa Mahakama ya rufaa mnamo Januari 2012, ana uzoefu wa miaka ishirini na sita kama mtaalam wa sheria,Jaji wa Mahakama Kuu na kama Jaji wa Mahakama ya Rufaa.

Mbele ya tume ya huduma za mahakama JSC Koome amesema kuwa iwapo atateuliwa kuwa jaji mkuu, atashirikiana na wadau husika katika idara ya mahakama ili kuweza kurekebisha uamuzi kuhusiana na hukumu ya kifo.

Aidha Jaji Koome amesema kuwa atahakikisha majaji 41 walioteuliwa na tume ya JSC wameapishwa ili kusaidia katika kutatua swala la mrundikano wa kesi mahakamani.

Jaji Koome alikuwa mmoja wa wanasheria ambao walishiriki kikamilifu katika juhudi za kufutwa kwa kifungu cha 2A cha Katiba ili kuhakikishia  mahakama uhuru wake.

Wengine wanaotafuta nafasi hiyo ni ikiwemo Jaji Juma Chitembwe aliyehojiwa siku ya jumatatu,Profesa Patricia Mbote aliyehojiwa hapo jana,Jaji David Marete Njagi,Wakili Phillip Murgor,Jaji Nduma Nderi,Wakili Fred Ngatia,Jaji William Ouko,Profesa Moni Wekesa pamoja na Wakili Alice Jepkoech Yano.

Nafasi hiyo ilibaki wazi baada ya jaji mkuu David Maraga kuustafu mapema mwakani huku naibu wake Philomena mwilu akiishikilia kikaimu.

 

Subscribe to eNewsletter