Highlights

Bunge la watoto lazinduliwa Marsabit kuimarisha ushiriki wa Watoto.

Na JB Nateleng

Bunge la watoto nchini Kenya (KCA) tawi la Marsabit limezinduliwa rasmi leo, hatua inayotajwa kuwa mwanzo mpya wa kuwahusisha watoto katika masuala yanayowahusu.

Uzinduzi huo unatarajiwa kutoa jukwaa kwa watoto kushiriki kikamilifu katika mijadala ya sera na sheria, pamoja na kutoa maoni yao katika masuala yanayowaathiri moja kwa moja.

Akizungumza na wanahabari, Afisa wa Masuala ya Watoto kaunti ndogo ya Marsabit Central, Leakey Mukanzi, amesema kuwa hatua hiyo itawapa watoto nafasi ya kushiriki katika maamuzi na kuchangia katika uundaji wa sera zinazolenga kuboresha maisha yao.

Mukanzi pia amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wadau na mashirika yanayotetea haki za watoto ili kuhakikisha bunge hilo linafanikiwa na kuchangia kulinda haki za watoto, pamoja na kupunguza visa vya dhuluma za kijinsia.

Kauli hiyo imeungwa mkono na Mary Nasibo, afisa wa programu za watoto katika shirika la FH Marsabit, ambaye amesema kuwa bunge hilo litawawezesha watoto kujieleza na kushiriki katika maamuzi yanayowahusu.

Hata hivyo, ametaja upana wa kaunti ya Marsabit kuwa changamoto katika kuwafikia watoto wengi ili waweze kushiriki kikamilifu katika mpango huo.

Post Comment