Askofu Kihara awataka wazazi na viongozi wawe mfano bora kwa Gen Z
Na Samuel Kosgei
Askofu wa Jimbo Katoliki la Marsabit, Mhashamu Peter Kariuki, amewataka wazazi, walimu, wahubiri na viongozi kuwa mfano mwema kwa kizazi cha sasa cha Gen Z, akisema vijana wengi wanakabiliwa na changamoto mbalimbali za maisha na wanahitaji kuongozwa badala ya kulaumiwa.
Akihubiri wakati wa misa katika Kanisa Katoliki la Maria Consolata mjini Marsabit, Askofu Kariuki alisema waumini wana wajibu wa kujadili hatma ya vijana na kuwalea kwa maadili mema, kama walivyofanya wamishonari walioanzisha Kanisa na taasisi za elimu zilizoweka msingi imara wa maendeleo katika jamii za wafugaji.
Askofu huyo pia amezitaka jamii za wafugaji kuwapeleka watoto wao shuleni badala ya kuwapeleka kuchunga mifugo. Alisisitiza kuwa vijana hawapaswi kulaumiwa wanapopoteza mwelekeo, kwani ni jukumu la watu wazima kuwapa mwongozo, kuwasikiliza na kuwa mfano bora. Aliongeza kuwa elimu ndiyo njia muhimu ya kubadilisha maisha ya jamii za wafugaji.
Akikumbuka mchango wa Wamishonari wa Consolata na wengine katika maendeleo ya Marsabit, Askofu Kariuki alisema si jambo la busara kwa wazazi kuwanyima watoto elimu ilhali wamishonari walijitolea kuanzisha shule na kuweka msingi madhubuti wa maendeleo kupitia elimu.
Wakati huohuo, aliwataka wananchi kuwachagua viongozi waadilifu wenye maslahi ya wananchi mioyoni mwao. Pia aliwahimiza waumini kuendelea kuliombea taifa na Kaunti ya Marsabit ili kudumisha amani, umoja na mshikamano.
Akizungumzia uchaguzi mkuu unaotarajiwa mwakani, Askofu Kariuki amewataka viongozi wa sasa na watakaochaguliwa kuongoza kwa uadilifu na kuwa chanzo cha matumaini kwa wananchi.



Post Comment