Local Bulletins

Jamaa mmoja akamatwa Wamba kwa madai ya kuiba ngamia wawili kutoka Laisamis

Na Henry Khoyan

Mtu mmoja anayedaiwa kuwa mwizi wa ngamia wawili walioibiwa katika eneo ya Laisamis siku chache zilizopita amepatikana.

Akithibitisha kisa hicho Naibu Chifu wa Nairibi, Alfred Lemasarit, ambaye kwa sasa ni kaimu Chifu wa Laisamis amesema jamaa huyo pamoja na ngamia walipatikana eneo la Wamba kaunti ya Samburu na sasa wako njiani kupelekwa Laisamis kwa hatua zaidi za kisheria.

Naibu huyo wa chifu ametoa wito kwa vijana kuacha tabia ya wizi wa mifugo na badala yake kujikita katika shughuli za maendeleo kama vile kuanzisha vikundi vya ushirika (saccos), kujiunga na vyuo vya kiufundi na kufanya kazi kwa bidii ili kuboresha maisha yao.

Zaidi ya hayo, chifu Lemasarit  ameomba mashirika yasiyo ya kiserikali kusaidia vijana hao katika kuboresha tabia zao na kuwapa msaada wa kielimu na kiuchumi.

Aidha ametoa wito kwa wazazi wote jimboni kuwa waangalifu zaidi na kufuatilia mienendo ya watoto wao wakati huu wa likizo fupi muhula wa kwanza.

Amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha watoto hawaingii katika shughuli au vitendo vinavyoweza kuwaathiri vibaya.

Chifu ameeleza wasiwasi wake juu ya hatari ambazo watoto wanaweza kukutana nazo wakiwa huru na bila usimamizi wa karibu.

Subscribe to eNewsletter