Local Bulletins

Wazazi jimboni Marsabit watakiwa kuwa waangalifu ili kuwaepusha wanao na utumizi wa mihadarati na dawa za kulevya.

Na Caroline Waforo,

Huku wanafunzi wakiendelea na mapumziko mafupi ya muhula wa kwanza wazazi wametakiwa kuwa waangalifu ili kuwaepusha wanao na utumizi wa mihadarati na dawa za kulevya haswa baada ya kubainika kuwa kiwango cha utumizi wa mihadarati kimeungezeka katika kaunti ya Marsabit.

Ni wito ambao umetolewa na afisa wa watoto katika eneo bunge la Saku Mukanzi Leakey ambaye amezungumza na Shajara ya Radio Jangwani afisini mwake.

Mukanzi ametoa wito kwa mamlaka ya kitaifa ya kupambana na dawa za kulevya nchini NACADA  kujenga afisi zake katika jimbo hili la Marsabit ili kufanikisha vita dhidi ya mihadarati na pombe haramu.

Afisa huyu wa watoto pia amewarai wazazi kuwaepusha watoto na kazi za sulubu kwani ni ukiukaji wa haki za watoto kulingana na sheria za taifa hili.

Vilevile wazazi wametakiwa kuhakikisha kuwa wanao hawajihusishi na shughuli za huduma za bodaboda kinyume na sheria.

Mapema wiki hii kamanda wa polisi katika kaunti ya Marsabit Leonard Kimaiyo pia aliwaonya vikali walanguzi wa dawa za kulevya kuasi biashara hiyo au wakabiliwe kisheria.

Kauli yake ikijiri wakati idara ya usalama inaendelea na msako dhidi ya walanguzi wa mihadarati na pombe haramu hapa jimboni Marsabit.

Subscribe to eNewsletter