Local Bulletins

Wazazi kaunti ya Marsabit watakiwa kuwapa wanao mafunzo ya kompyuta baada ya shule ya pili….

Na Isaac Waihenya,

Wazazi katika kaunti ya Marsabit wametakiwa kuhakikisha kwamba wanao wamepata mafunzo ya kompyuta haswa baada ya kukamilisha kidato cha nne ili kuwapa ujuzi wa kidijitali.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa kituo cha kuwawezesha vijana cha Ebisa Youth Empowerment Center,Abdikadir Doyo Wario ni kuwa mafunzo hayo yatawapa vijana ujuzi utakaowawezesha kujiajiri au hata kupiga hatua katika masomo yao katika tasisi za elimu ya juu.

Akizungumza kwenye hafla ya kufunzu kwa wanafunzi 89 waliohitimu katika mafunzo ya kompyuta katika kituo hicho cha kuwawezesha vijana cha Ebisa, hapa mjini Marsabit, Doyo Wario ameyataja mafuzo ya kompyuta kuwa muhimu kwa kila mmoja haswa wakati huu ambapo ulimwengu umepiga hatua kidijitali.

Aidha Doyo Wario amesema kuwa changamoto wanazopitia vijana katika kaunti ya Marsabit ikiwemo ukosefu wa tajiriba ya kompyuta haswa wakati wa kusaka ajira au kuendeleza shuguhuli zao za kila siku, kama iliyomchochea yeye kuanzisha mafunzo hayo ili kuwainua vijana hapa jimboni.

Baadhi ya wazazi wa wanafunzi waliohitimu wamepongeza hatua hiyo huku wakiitaja kama itakayowasaidia wakati wa kusomea kozi zingine watakazo katika vyuo vikuu au tasisi zingine za elimu ya juu.

Hata hivyo baadhi ya wanafunzi walionufaika na mafunzo hayo ya kompyuta wametaja kwamba yatawafaidi katika maisha yao ya usoni, huku wakiwarai viongozi wengine jimboni kuiga mfano wa kituo hicho cha kuwawezesha vijana cha Ebisa.

Subscribe to eNewsletter