Local Bulletins

NDMA yasema kuwa familia 109,000 jimboni Marsabit zinahitaji msaada wa chakula.

Na Caroline Waforo

Visa vya utapiamlo vimeongezeka hadi asilimia 17 kutoka asilimia 13.5 katika kaunti hii ya Marsabit.

Ongezeko hili likiwa ni kutoka mwezi Julai mwaka jana hadi sasa.

Hii ni kulingana na afisa mkuu wa lishe bora jimboni David Buke ambaye amezungumza na shajara ya radio Jangwani wakati wa mkutano wa kuangazia majanga yanayokumba jimbo la Marsabit ulioandaliwa leo Jumatano.

Buke ameweka wazi kuwa Maeneo bunge ya Northhorr na Laisamis yanaendelea kuongoza katika visa hivyo. Aidha visa hivi vimetajwa kuwa juu katika wadi za Golbo, Sololo, Marsabit Central kati ya wadi zingine jimboni.

Vilevile visa hivi vinashuhudiwa katika miji iliyo humu jimboni Marsabit.

Watoto wadogo na akina mama ndio wameathirika pakubwa na visa hivi vya utapiamlo.

Ongezeko la visa hivi ni kutokana na ugumu wa maisha pamoja na kiangazi kinachoendelea kushuhudiwa kwa sasa.

Buke amesema kuwa maafisa wa afya wanaendelea kufanya uchunguzi kule mashinani huku pia akiwarai wazazi kuhakikisha kuwa wanawapeleka wanao katika vituo vya afya ili kupata virutubishi vya aina mbalimbali.

Mapema mwezi huu mamlaka ya kutathmini hali ya ukame nchini NDMA tawi la Marsabit ilisema kuwa familia 109,000 jimboni Marsabit zinahitaji msaada wa chakula. Hii ikiweka jamii katika hatari ya hali ya utapiamlo

 

 

Subscribe to eNewsletter