Marehemu padre Frank atajwa kama mtu mkarimu aliyependa kusaidia wasiojiweza katika jamii.
January 22, 2025
Na Samuel Kosgei
Marehemu Padre Francisco Terragni ametajwa kama mtu mkarimu aliyependa kusaidia maskini na wasiojiweza kwa namna moja ama nyingine katika jamii.
Padre mkuu wa parokia ya Dirib Gombo Fr George Guyo amesema kuwa marehemu Frank aliishi maisha ya chini na ya unyenyekevu bila kubagua hali ya mtu yeyote.
Amemumiminia sifa akisema kuwa alipenda kutagusana na watu wa chini na kufanya sala kwa sana bila kukosa kushiriki misa.
Aidha amesema kwa marehemu padre Frank alipenda kujitolea kujengea makao watu ambao hawakuwa na uwezo kijijini sawa na kukarabati barabarani akitumia hela zake.
Wengine waliomjua Fr Frank akiwemo Sista Mary Auma amesema kuwa marehemu alikuwa mtu aliyependa sana kuhubiri injili bila kusuasua katika Imani.
Katekista Philip Waqo kutoka kanisa katoliki la Badasa parokia ya Dirib Gombo amesema kuwa padre Frank alikuwa na uhusiano mzuri na watoto na makatikista.
Baba Askofu Peter Kihara amesema kwamba misa ya Mazishi itafanyika kesho Alhamisi katika kanisa la cathedral mjini Marsabit kuanzia saa nne asubuhi.
Padre Francisco alizaliwa tarehe 25/03/1943 katika taifa la Italia na kupokea upadrisho katika taifa la Congo, Jimbo la Bukavu.
Padre Francisco ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 81.
Alihudumu katika Parokia ya Sololo kuanzia mwaka wa 2006-2007, Parokia ya Moyale mnamo mwaka wa 2007-2010 kisha akahudumu katika Parokia ya Dirib Gombo kuanzia mwaka wa 2010 hadi wakati wa kifo chake.
Raha ya milele umpe ee bwana na Mwanga wa milele umwangazie, apumzike kwa amani.