Marehemu padre Frank atajwa kama mtu mkarimu aliyependa kusaidia wasiojiweza katika jamii.
January 22, 2025
Jimbo katoliki la Marsabit linasikitika kutangaza kifo cha Padre Francisco (Frank) Terragni kilichotokea tarehe 17 Januari 2025 katika Hospitali ya Huruma kule Nanyuki
Akidhibitisha taarifa hiyo Askofu wa Jimbo Katoliki la Marsabit Mhashamu Baba Askofu Peter Kihara amesema kwamba mwili wa marehemu utawasili na kupokelewa Marsabit hii leo tarehe 22 Januari 2025 kwa ibada ya misa ya wafu katika kathedrali ya jimbo la Marsabit mnamo mida ya saa kumi alasiri.
Baba Askofu amesema kwamba misa ya Mazishi itafanyika kesho Alhamisi tarehe 23/1/2025 katika Kathedrali ya Marsabit kuanzia saa nne asubuhi.
Padre Francisco alizaliwa tarehe 25/03/1943 katika taifa la Italia na kupokea upadrisho katika taifa la Congo, Jimbo la Bukavu.
Padre Francisco ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 81.
Alihudumu katika Parokia ya Sololo kuanzia mwaka wa 2006-2007, Parokia ya Moyale mnamo mwaka wa 2007-2010 kisha akahudumu katika Parokia ya Dirib Gombo kuanzia mwaka wa 2010 hadi wakati wa kifo chake.
Mapadre katika Jimbo Katoliki la Marsabit wamemmiminia sifa mwendazake Padre Francisco.
Akizungumza na idhaa hii Baba paroko wa parokia ya Maria Consolata Kathedrali Titus Makokha amemtaja Padre Francisco kama Padre mcha mungu aliyewapenda watu wote bila ubaguzi wala mapendeleo.
Raha ya milele umpe ee bwana na Mwanga wa milele umwangazie, apumzike kwa amani.