Local Bulletins

Idara ya maji Marsabit yaahidi kukabiliana na utata unaozunguka kero la maji

Na Caroline Waforo

Idara ya maji jimboni Marsabit imelalamikia utata unaozunguka usimamizi wa miradi ya maji jimboni.

Hii ni kutokana na ufujaji mkubwa wa fedha unaoshuhudiwa katika kamati za usimamizi wa miradi hiyo zinazotawaliwa na watu wanaosemekana kuwa makateli.

Akizungumza na shajara ya radio Jangwani leo Jumatatu waziri wa maji katika kaunti ya Marsabit Grace Galmo amelaumu baadhi ya wabunge jimboni kwa kuingilia usimamizi wa miradi hiyo.

Waziri Galmo amelitaja hilo kuwa changamoto kuu huku akiahidi kuwa idara yake italainisha usimamizi wa maji jimboni kwa kuhusisha jamii kupitia ushirikishwaji wa umma.

Aidha waziri Galmo amesema kuwa iwapo miradi hii itasimamiwa ipasavyo wakaazi jimboni wanaweza kunufaika pakubwa.

Hata hivyo waziri Galmo amedokeza kuwa idara yake imeweka mikakati ya kusajili visima vyote jimboni kihalali.

Kauli ya waziri imeungwa mkono na mkurugenzi wa idara ya maji jimboni Boku Sharamo ambaye ameweka wazi kuwa wanakabiliana na changamoto hiyo.

Akizungumza wiki jana katika mkutano moja uliowaleta pamoja wadau mbalimbali wa idara ya maji katika eneo bunge la moyale kaunti ya Marsabit gavana wa kaunti ya Marsabit Mohamud Ali ambaye pia anaunga mkono hatu za kulainisha usimamizi wa maji jimboni, aliahidi kuzima makateli hao.

Haya yanajiri huku uhaba wa maji ukiendelea kushuhudiwa jimboni Marsabit kutokana na kiangazi kinachoshuhudiwa kwa sasa.

Mamlaka ya kutathmini hali ya ukame nchini NDMA tawi la Marsabit ikisema kuwa wakaazi jimboni wanahitaji maji kwa dharura.

Subscribe to eNewsletter