Local Bulletins

MAHAKAMA YAKATAA KUZUIA BUNGE LA SENETI KUSKIZA KESI YA GACHAGUA

Naibu Rais Rigathi Gachagua, amepata pigo lingine baada ya Mahakama Kuu kukataa kuzuia Seneti isisikilize hoja ya kumng’oa mamlakani.

Hii inamaanisha kwamba Gachagua atajitetea dhidi ya tuhuma zilizowasilishwa kama msingi wa kumng’oa mamlakani wakati hoja hiyo itakapowekwa mbele ya Seneti siku ya Jumatano na Alhamisi, kulingana na mpango uliopo.

Jaji Chacha Mwita wa Mahakama za Milimani, katika uamuzi wake, alisema kwamba mchakato wa kumng’oa mamlakani unapaswa kuendelea hadi mwisho wake.

Jaji Mwita pia amemtaka Jaji Mkuu Martha Koome kuipa jopo la majaji watatu liloundwa kusikiliza na kuamua kesi hiyo.

Jaji Mkuu Koome tayari ameunda jopo linaloongozwa na Jaji Erick Ogola, Antony Mrima na Dr. Frida Mugambi, kusikiliza maombi matano yanayotaka kuzuia kumng’oa Naibu Rais Gachagua.

Wiki iliyopita bunge la kitaifa lilipiga kura ya kumng’atua afisini Naibu Rais kwa kukiuka sheria.

 

Subscribe to eNewsletter