Highlights

Wito watolewa kuboresha mazingira ya elimu kwa wanafunzi, Marsabit

Na JB Nateleng

Wito umetolewa kwa serikali ya kitaifa, serikali ya kaunti ya Marsabit na wadau mbalimbali wa elimu kuhakikisha kila mwanafunzi shuleni anapata maji safi, huduma bora za afya na mazingira salama ya kujifunzia ili kuboresha kiwango cha elimu katika jimbo la Marsabit.

Wito huo umetolewa wakati wa maadhimisho na uzinduzi wa kitaifa wa Siku ya mtoto wa Afrika uliofanyika katika Shule ya Msingi ya SKM, eneo bunge la Saku.

Akizungumza katika hafla hiyo, Gavana wa bunge la watoto Kenya (KCA) tawi la Marsabit na ambaye pia ni mwanafunzi wa shule ya upili ya Cavallera Girls, Gumato Barille Wario, amesema kuwa ukosefu wa maji safi ni miongoni mwa changamoto kuu zinazowakabili wanafunzi wengi na kuathiri uwezo wao wa kuzingatia masomo.

Gumato amewataka viongozi wa serikali za kitaifa na kaunti kushirikiana katika kubuni mikakati madhubuti ya kushughulikia changamoto zinazowakabili watoto wa Marsabit, akisema wengi wao wana ndoto kubwa zinazohitaji mazingira bora ili kuzifikia.

Kwa upande wake,Halkano Wako ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Upili ya Saku, ameitaka jamii kuachana na mila potovu kama vile ukeketaji na ndoa za utotoni, akisema desturi hizo zinaendelea kuathiri elimu na mustakabali wa mtoto wa kike.

Siku ya mtoto wa Afrika huadhimishwa kila mwaka Juni 16 ili kuwaenzi wanafunzi waliouawa wakati wa Machafuko ya Soweto ya 1976 nchini Afrika Kusini.

Hafla hii inatumika kutetea haki za watoto, kudai upatikanaji bora wa elimu, na kushughulikia changamoto za kila siku za vijana katika bara la Afrika.

Post Comment