Highlights

Ukeketaji, ndoa za utotoni na mimba za mapema bado tishio kwa watoto Marsabit, asema kamishna.

Na Samuel Kosgei

KAMISHNA wa Kaunti ya Marsabit, Stanley Kamande, amezitaka jamii za eneo hili kuachana na mila na desturi zinazochangia ukeketaji wa wasichana, ndoa za utotoni na mimba za mapema.

Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika katika Shule ya Msingi ya SKM, Kamande alisema changamoto hizo tatu ndizo zinazochangia kwa kiwango kikubwa kudorora kwa maendeleo na ustawi wa watoto katika kaunti hii.

Amesema ofisi yake itaendelea kuimarisha juhudi za kupambana na vitendo hivyo kwa kuwa vinaathiri haki za watoto, hususan upatikanaji wa elimu.

CUE IN… STANLEY KAMANDE

Kamande pia alieleza wasiwasi kuhusu idadi kubwa ya watoto wanaokosa kuendelea na masomo baada ya kumaliza elimu ya msingi, hali inayokwenda kinyume na azma ya serikali ya kuhakikisha asilimia 100 ya wanafunzi wanajiunga na shule za sekondari.

Alisema wavulana ndio wanaoathirika zaidi na tatizo la kuacha shule ikilinganishwa na wasichana. Kulingana naye, baadhi ya wavulana huondolewa shuleni na kutumwa kuchunga mifugo, jambo linalowanyima haki yao ya kupata elimu.

CUE IN… BOY CHILD

Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika hufanyika tarehe 16 Juni kila mwaka kwa kumbukumbu ya wanafunzi waliouawa katika maandamano ya Soweto nchini Afrika Kusini mwaka 1976 wakidai haki ya kupata elimu bora.

Mwaka huu, maadhimisho hayo yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Kuhakikisha upatikanaji wa maji safi, huduma za usafi wa mazingira na usafi binafsi kwa kila mtoto barani Afrika,” ikilenga kuhamasisha serikali na wadau mbalimbali kuboresha huduma za maji na usafi kwa watoto kote barani.

Post Comment