Highlights

Wakazi walalamikia daraja bovu Shauri Yako Marsabit.

NA Nyabande Orwa

Wakazi wa Shauri Yako katika eneo bunge la Saku, kaunti ya Marsabit, wamelalamikia ubovu wa madaraja ya Elisha Godana na Abawama.

Wakizungumza na kituo hiki, wakazi hao wamewakosoa viongozi wa kaunti kwa kushindwa kuyakarabati madaraja hayo licha ya muda mrefu kupita baada ya kuporomoka.

Kiongozi wa vijana Abdiaziz Boru amesema kuporomoka kwa madaraja hayo kumeathiri shughuli za kila siku kwenye maeneo hayo. Ameongeza kuwa kina mama wajawazito na wanafunzi wako hatarini hasa wakati wa mvua.

Boru ametoa wito kwa idara za KeRRA na KURA pamoja na uongozi wa kaunti kushirikiana ili daraja hilo litengenezwe haraka kabla ya kufunguliwa kwa muhula wa pili wa shule.

Wakati huo huo, wazee wa Manyatta ya Shauri Yako wameeleza hofu kuhusu usalama na uwezekano wa mlipuko wa magonjwa, baada ya baadhi ya wakazi kuanza kutupa taka kwenye laga hiyo.

Wamesema maji yanayotiririka katika eneo hilo yanatumiwa na wakazi wa maeneo ya chini, jambo linaloweza kuhatarisha afya yao.

Wazee hao sasa wanaitaka serikali kuchukua hatua za haraka kukarabati daraja hilo ili kuepusha janga.

Kwa mujibu wa wakazi, ukarabati wa daraja hilo utasaidia kuunganisha maeneo ya Drip Gombo, Sagante na Badassa.

Post Comment