Highlights

Serikali kusambaza chakula cha mifugo kukabili ukame Kaskazini Mashariki asema waziri Ruku.

NA Nyabande Orwa

Serikali imeanzisha mchakato wa kusambaza chakula cha mifugo katika maeneo yaliyoathirika pakubwa na ukame, hususan katika kaunti za Kaskazini Mashariki mwa nchi.

Hayo yamesemwa na waziri wa utumishi wa umma, Geoffrey Ruku, alipokuwa akizungumza na kituo hiki wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa vyumba vya kulala vya wanafunzi katika chuo cha mafunzo ya ufundi na stadi cha North Horr, kwa mwaliko wa mbunge wa eneo hilo, Wario Adhe.

Ruku amesema kupitia mpango wa serikali, mifugo iliyoathirika zaidi itapatiwa chakula ili kuzuia vifo vinavyoweza kusababishwa na kiangazi kirefu, huku hatua hizo zikizingatia hali ya mazingira katika kila kaunti.

Wakati huo huo, Waziri huyo amesema serikali inaendelea kuweka mikakati ya kuboresha upatikanaji wa maji katika kaunti za Kaskazini Mashariki kama njia ya kudhibiti tatizo la muda mrefu la uhaba wa maji.

Aidha, Ruku amesema kupitia Shirika la Kitaifa la usimamizi wa mazingira, NEMA, serikali inakabiliana na mmea vamizi wa Mathenge ambao umeharibu mazingira na kupunguza maeneo ya malisho.

Miongoni mwa viongozi waliohudhuria hafla hiyo ni Katibu wa kanda kutoka Idara ya makazi, Polycarp Onyango, na Mkurugenzi Mkuu wa NEMA, Mamo B. Mamo.

Post Comment