Ngurunit kuadhimisha mwaka mmoja wa parokia mwishoni mwa wiki.
Na JB Nateleng
Tangu kuanzishwa kwa parokia ya Ngurunit katika Jimbo katoliki la Marsabit mnamo Juni 24 mwaka jana, waumini wa kanisa katoliki katika eneo hilo wameendelea kunufaika na huduma za kiroho, mafunzo ya imani na huduma mbalimbali za kanisa karibu na makazi yao.
Katika kipindi cha mwaka mmoja, parokia hiyo imeshuhudia ukuaji wa imani, huku idadi ya waumini ikiendelea kuongezeka na wengi zaidi wakilikumbatia neno la Mungu.
Akizungumza na Shajara ya Radio Jangwani kwa njia ya simu, baba paroko wa Ngurunit, Padri Martin Ndumia, amesema idadi ya familia za kikristo imeongezeka kutoka 52 hadi 80, jambo linaloonyesha maendeleo ya uinjilisti katika eneo hilo.
Padri Martin amesema changamoto kubwa zinazoikabili parokia hiyo ni ukubwa wa eneo linalohudumiwa pamoja na ubovu wa miundombinu, hali inayofanya iwe vigumu kuwafikia waumini wanaoishi katika maeneo ya mbali.
Licha ya changamoto hizo, ameupongeza ushirikiano uliopo kati ya viongozi wa kidini na wakazi wa Ngurunit, akisema umechangia kuimarisha shughuli za uinjilisti na kukuza imani ya Kikatoliki katika eneo hilo.
Aidha, Padri Martin amewaalika waumini wote wa Jimbo katoliki la Marsabit kushiriki maadhimisho ya mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwa Parokia hiyo, yatakayofanyika Julai 5, 2026.



Post Comment