Naibu mwenyekiti wa kamati ya amani Adan Chukulisa atoa wito wa amani, Marsabit huku akikashifu matamshi ya hivi punde ya Rigathi Gachagua
NA Joseph Muchai
Naibu mwenyekiti wa kamati ya amani katika kaunti ya Marsabit Adan Chukulisa amewahimiza wananchi jimboni kuendelea kudumisha amani na kutokubali kutenganishwa kwa misingi ya kikabila wala kisiasa hasa wakati huu taifa linapoelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Marsabit Chukulisa amewataka wananchi kujitenga na viongozi wanaoeneza siasa za chuki akisema kuwa baadhi yao hutumia siasa za migawanyiko kwa manufaa yao binafsi.
Vilevile, amekashifu matamshi ya aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua aliyedai kuwa viongozi wa Kaskazini mwa nchi hawafanyi maendeleo katika maeneo yao.
Chukulisa amesema kuwa kaunti za Kaskazini zimekuwa zikitengwa kimaendeleo huku akidai kuwa matamshi ya Gachagua ni ya kuchochea migawanyiko miongoni mwa jamii.
Na huku athari za kiangazi zikiendelea kushuhudiwa jimboni Chukulisa ameirai serikali pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali kuingilia kati na kutoa misaada kwa wakaazi wanaokabiliana na makali ya njaa.



Post Comment