Hospitali ya uzazi yazinduliwa Lontolio Kuboresha Huduma ya afya kwa Akina Mama
Wakazi wa eneo la Lontolio katika Eneo Bunge la Laisamis sasa wanatarajia kupata huduma bora za uzazi baada ya kuzinduliwa kwa hospitali mpya ya uzazi iliyojengwa kwa ufadhili wa kampuni ya Lake Turkana Wind Power.
Hospitali hiyo, iliyogharimu shilingi milioni 23, inalenga kupunguza changamoto ambazo akina mama walikuwa wakikumbana nazo kwa kusafiri hadi mji wa Laisamis ili kujifungua.
Meneja wa Uhusiano na Jamii wa Lake Turkana Wind Power, Job Lengoyap, amesema hospitali hiyo ni mradi wa 104 ambao kampuni hiyo imekamilisha katika Eneo Bunge la Laisamis. Ameeleza kuwa kampuni inalenga kuimarisha huduma za afya katika jamii.
Job pia amewahimiza akina mama wa Eneo Bunge la Laisamis kujifungulia hospitalini. Amenukuu ripoti ya Wizara ya Afya inayoonyesha kuwa kati ya wanawake 106 wanaojifungua kila mwaka katika eneo hilo, ni wanawake 40 pekee wanaojifungulia hospitalini.
Afisa wa Uhusiano na Jamii wa Lake Turkana Wind Power, Mohammed Samana, amesema walijenga hospitali hiyo Lontolio kwa sababu kijiji hicho kipo katikati ya vitongoji vya eneo hilo, hivyo kituo hicho kitawahudumia pia wakazi wa vijiji jirani.
Muuguzi Mkuu wa hospitali hiyo, Antonella Lekupez, amesema kituo hicho kitaboresha huduma za afya na kupunguza changamoto ambazo wakazi, hasa akina mama wajawazito, walikuwa wakikumbana nazo wanapotafuta huduma za matibabu.
Hata hivyo, ameomba wahisani kusaidia kuajiri mlinzi wa kituo hicho, kujenga uzio na kuongeza idadi ya wahudumu wa afya.
Mkuu wa Idara ya Afya katika Kaunti Ndogo ya Laisamis, Yusuf Galmogle, amesema hospitali hiyo itahudumia zaidi ya wakazi 2,335 wa eneo hilo. Ameongeza kuwa idara yake itaendelea kushirikiana na Lake Turkana Wind Power ili kuboresha huduma za afya na maisha ya jamii.



Post Comment