Gavana wa Marsabit Mohamud Ali aitaka serikali kuu kuharakisha mchakato wa kutoa misaada ya chakula kwa wakazi wa kaskazini mwa nchi.
NA SAMUEL KOSGEI
Gavana wa Marsabit Mohamud Ali leo amefanya kikao na Katibu katika wizara ya Programu Maalum za Serikali Kuu, Ismail Maalim ili kujadili hali ya ukame inayoendelea katika Kaunti ya Marsabit, ambayo ni miongoni mwa kaunti 23 za eneo-kame zinazoathirika kwa sasa.
Kwenye taarifa yake kwenye mtandao wa facebook gavana Ali amesema kuwa amemwarifu Katibu Ismail kuhusu athari za ukame wa muda mrefu kwa jamii zinazoishi kaskazini mwa nchi.
Aidha anasema kuwa kuna haja ya dharura ya kuimarisha hatua za pamoja na zilizoratibiwa ili kuwakinga wananchi kutokana na makali ya njaa.
Amesema Serikali ya Kitaifa kupitia Idara ya Programu Maalum imemwakikishia msaada kwa dhamira thabiti ya kuokoa maisha, kulinda riziki, na kuhakikisha hakuna mtu anayeachwa nyuma.
Ameongeza kuwa kwa dharura serikali yake itaongeza misaada ya chakula cha dharura, usambazaji wa maji kwa malori, pamoja na hatua nyingine za haraka, sambamba na mikakati ya muda mrefu ya kupunguza athari za ukame.



Post Comment