FH yaadhimisha miaka 50 ya huduma kwa jamii Marsabit
Na Nyabande Orwa
Shirika lisilo la kiserikali la Food for the Hungry (FH) limeadhimisha miaka 50 ya huduma kwa jamii katika hafla iliyofanyika katika shule ya AIC compassion Karare, eneo ambalo lilikuwa miongoni mwa sehemu za mwanzo za shughuli za shirika hilo.
Katika hotuba yake iliyosomwa na meneja wa programu wa FH Marsabit, Dkt. Abdub Golicha, mkurugenzi mkuu wa FH Kenya, Ann Karau, amesema kuwa simulizi za mafanikio kutoka kwa walionufaika na miradi ya shirika hilo zinawapa motisha wa kuendelea kuwahudumia wananchi wenye mahitaji mbalimbali.
Karau pia ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na FH ili kuhakikisha kuwa huduma zinawafikia watu wengi zaidi wanaohitaji msaada katika jamii.
Wakati huo huo, mgeni wa heshima katika hafla hiyo ambaye ni waziri wa jinsia katika kaunti ya Marsabit, Armara Galwab, amesema kuwa FH imetekeleza miradi yenye manufaa makubwa katika kaunti hii, ikiwemo kuboresha elimu mashuleni, kusambaza huduma za maji, kusaidia watoto wanaotoka katika familia zisizojiweza, pamoja na kutoa mafunzo ya lishe kwa akina mama katika maeneo ya mashinani.
Kwa upande wao, baadhi ya walionufaika na ufadhili wa masomo kutoka FH wameeleza shukrani zao kwa shirika hilo, wakisema lilisimama nao wakati walipokuwa hawana uwezo wa kuendelea na masomo. Wamesema bila msaada huo, huenda wasingefikia mafanikio waliyonayo leo.



Post Comment