County Updates, Diocese of Marsabit, Local Bulletins

Afueni kwa wagonjwa katika hospitali za rufaa za Marsabit baada ya serikali kupokea dawa kutoka kwa mamlaka ya kusambaza dawa nchini KEMSA.

Waziri wa afya katika kaunti ya Marsabit Grace Galmo. Picha; Samuel Kosgei

Na Samuel Kosgei,

Huenda sasa ikawa afueni kwa wagonjwa katika hospitali za rufaa za Marsabit baada ya serikali kupokea dawa kutoka kwa mamlaka ya kusambaza dawa nchini KEMSA.

Akizungumza baada ya kupokea dawa hizo katika hospitali ya rufaa ya Marsabit, waziri wa afya Grace Galmo amesema kuwa dawa hizo zimegharimu serikali shilingi milioni 46 na hivyo kuna haja ya wananchi sasa kupata matibabu hospitalini wanapougua.

Zahanati 53 kati ya 114 za mashinani zitapokea dawa hizo huku nyingine pia zikipokea dawa hizo kuanzia wiki ijayo.

Amekariri kuwa wizara yake itarekebisha hali ya hospitali za umma mashinani ili kuimarisha afya ya wananchi wa chini.

Ameitika bunge la kaunti kuongeza mgao wa pesa kwenye wizara ya afya kwani kulingana naye mgao wa wizara yake iko chini ya matarajio kwani wamekuwa wakipiga bajeti ya shilingi millioni 280 kwa mwaka kinyume na sh.90m wanazopata kwa sasa.

Afisa mkuu mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Marsabit Kusu Abduba amehakikishia wananchi kuwa karne ya dawa za hospitali kuibiwa na kuuzwa nje umeisha kwani uongozi wake umeweka mikakati mwafaka wa kuzuia matukio kama hayo.

Afisa mkuu mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Marsabit Kusu Abduba. Picha; Samuel Kosgei

Naibu katibu katika ofisi ya gavana Tari Doti amekariri haja ya dawa hizo kulindwa ili kusaida wananchi haswa wakti huu ambapo kiangazi kinashuhudiwa na magonjwa mengi kujitokeza.

Subscribe to eNewsletter