County Updates, Diocese of Marsabit, Local Bulletins

Wanafunzi Wa Shule Ya Msingi Ya Elmollo Iliyo Eneo La Loiyangalani Wahangaika Kufika Shuleni Baada Ya Barabara Kusombwa Na Maji.

Picha;Hisani

By Adho Isacko

Kufuatia kuongezeka kwa viwango vya maji katika eneo la Loiyangalani kaunti ya Marsabit mwaka jana shule kadhaa zimeadhirika huku barabara zikikatika na vyoo pamoja na madarasa kuzama.

Katika shule ya msingi ya Elmollo iliyo eneo la Loiyangalani wanafunzi sasa wanataabika hata kufika shuleni kwani barabara waliyokuwa wakitumia imesombwa na maji.

Akidhibitisha hayo mwalimu wa shule hiyo Richard Snaron amesema kuwa wanafunzi wengi wanakosa mahitaji ya kimsingi kama vile vyoo shuleni humo na pia uhaba wa walimu umekuwa changamoto kwani wizara ya elimu haiongezi walimu licha ya wao kutuma barua mara kwa mara.

Kulingana na mkurugenzi mkuu wa shirika lisilokuwa la kiserikali la KDEF Ahmed Kura, wengi wa wanafunzi katika shule ya msingi ya Elmolo na shule ya Santuru wanakosa vifaa vya kimsingi wakati huu ambapo shule zimefunguliwa. Kura amesema kuwa wanafunzi wengi kwa sasa wanakaa sakafuni ili waweze kufuatia maagizo ya wizara ya afya ya kukaa umbali wa mita moja unusu.

Aidha Kura amesema kwamba, maafisa wa elimu, naibu kaunti kamishna kwa ushirikiano na shirika la KDEF wanapania kuzunguka kaunti ya marsabit hasa maeneo ya mashinani kwa jumla ili kuwahimiza jamii kurudisha watoto shuleni kwani wengi wa wanafunzi bado hawajafika shuleni.

Ameongeza kuwa kama shirika wanawahimiza serikali ya kaunti pamoja na mashirika mengine ambayo yanasaidia wanafunzi kujumuika na kuhakikisha kwamba wanafunzi wote waliorudi shuleni wanakingwa dhidi ya korona.

Aidha, katika baadhi ya kaunti kama vile Baringo na Kisumu, baadhi ya shule ziliharibiwa na mafuriko na imelazimu madarasa kujengwa upya.

 

Subscribe to eNewsletter