Local Bulletins

ODM YATAKA SERIKALI IWAJIBIKIE MAUAJI, MAJERUHI NA UTEKAJI NYARA ULIOSHUHUDIWA NCHINI.

NA SAMUEL KOSGEI

Chama cha ODM kinachoongozwa na Raila Odinga kinaitaka serikali ya Kenya Kwanza kuwajibikia mauaji, majeruhi na utekaji nyara ulioshuhudiwa nchini kufuatia maandamano ya Gen Z kupinga mswada tata wa fedha.

Katika taarifa iliyosomwa na katibu mkuu wake Edwin Sifuna jijini Nairobi chama hicho kimeendelea kukashifu maafisa wa polisi kwa kutumia nguvu kupita kiasi kuwakabili waandamanaji na kupelekea maafa ya wakenya 39 kulingana na Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Binadamu nchini, KNCHR.

Aidha uongozi wa chama hicho umekosoa utekaji nyara wa wanaharakati huku wakidai kuwa zaidi ya watu 50 hawajulikani waliko.

Chama hicho pia kimeitaka Mamlaka Huru ya Kuangazia Utendakazi wa Polisi nchini, IPOA kufanya uchunguzi wa vifo vya waandamanaji pamoja na madai ya mauaji ya watu katika eneo la Githurai kaunti ya Kiambu.

Na huku rais akiendelea kutoa wito wa mazungumzo na vijana chama hicho kinasema kuwa rais hajaonyesha nia njema ya kushiriki mazungumzo hayo.

Aidha chama hicho kimekosoa matamshi ya rais Jumapili kwa kile kinasema ni kutishia kupunguza mgao wa fedha katika idara mbalimbali za serikali ikiwemo idara ya mahakama baada ya kutupiliwa kwa mswada tata wa fedha.

Chama hicho pia kimetangaza kuwa kitaongoza mchakato wa kuodolewa afisini kwa baadhi ya wabunge wa ODM waliopiga kura ya kuunga mkono mswada tata wa fedha kinyume na matarajo ya wananchi.

Wabunge hao ni kutoka maeneo bunge hayo ni pamoja na Gem Bondo, Navakholo, Kajiado Central, Ikolomani pamoja na Suba South.

Subscribe to eNewsletter