Supkem Marsabit yaunga mkono wito wa kuwajibisha serikali ya Kenya Kwanza.
December 5, 2024
Na Caroline Waforo
Maandamano ya Gen Z kaunti ya Marsabit yalikosa kufanyika hii leo kutokana na taarifa za kuingiliwa na wahuni kwa nia ya kusababisha uharibifu wa mali.
Kulingana na Kamanda wa kaunti ya Marsabit Leonard Kimaiyo kunao wahuni waliopanga kuvuruga maandamano hayo na kusababisha uharibifu.
Kamanda Kimaiyo anasema kuwa vijana waliokuwa wamepanga kushiriki maandamnao hayo walikubaliana na idara ya usalama kusitishwa kwa maandamano ili kuzuia uharibufu.
Aidha mapema leo Alhamisi baadhi ya vijana walichoma moto matairi karibu na shule ya upili ya Moi Girls japo walitawanywa na maafisa wa polisi waliokuwa wakishika doria mjini Marsabit.
Kulingana na notisi iliyokuwa imewasilishwa kwa OCS wa Marsabit Edward Mabonga vijana hawa walikuwa wakipanga kuwajibisha serikali ya kaunti ya Marsabit pamoja na ile ya kitaifa kupitia maandamano ya amani.
Gen Z wanaitaka serikali ya kaunti ya Marsabit inayoongozwa na Gavana Mohamud Ali kuwalipa wahudumu wa afya malimbikizi yao ya mishahara ya hata miezi minane, kuwalipa wafanyikazi wa kaunti mishahara yao ya miezi miwili pamoja na kutaka haki ya utoaji wa ajira jimboni.
Walidai kuwa asilimi 60 ya wafanyikazi wa kaunti ya Marsabit ni wakaazi kutoka kaunti nyingine nchini.
Katika Maswala ya kitaifa vijana hawa walitaka serikali kupunguza mishahara ya maafisa wa serikali ikiwemo rais, naibu wake, magavana, wabunge, maseneta, wawakilishi wa akina mama.
Maswala mengine ni serikali kutupilia mbali ushuru wa nyumba wa asilimia 1.5, kuteuliwa kwa makamishna wa tume huru ya uchaguzi IEBC kati ya maswala mengine.