Local Bulletins

Shule ya Upili ya wasichana ya Bishop Cavallera kaunti ya Marsabit yavamiwa na majambazi

Shule ya upili ya Bishop Cavallera, Kharare, Marsabit

By Machuki Dennson

Majambazi wamevamia shule ya upili ya Bishop Cavallera hapa Marsabit usiku wa kuamkia leo Ijumaa na kuiba ng’ombe kutoka shuleni humo.

Kulingana na mwalimu mkuu wa shule hiyo mtawa Sr. Regina Mutuku wezi hao walivamia shule hiyo mwendo wa saa mbili unusu wakiwa wamejihami na bunduki.

Sr. Mutuku anayesimamia shule hiyo inayomilikiwa na jimbo katoliki la Marsabit amesema ng’ombe wote wanane waliokuwa shuleni wamechukuliwa.

Hata hivyo kwa bahati nzuri hakuna mwanafunzi au mtu aliyejeruhiwa kufuatia kisa hicho.

Juhudi za polisi kuwafuata ng’ombe hao usiku huo hazijafua dafu maana hadi kufikia sasa bado mifugo hao hawajarejeshwa shuleni.

Mlinzi wa  shule anasema kuwa aliwaona wezi wanne katika lango la shule hiyo na wengine zaidi wakiwa wamezingira. Kati ya wanane hao sita walikuwa na bunduki na walipiga risasi wakiingia shuleni. Askarirungu ameiambia Radio Jangwani kuwa waliweza kuwaokoa mbuzi watano pekee japo ng’ombe wote watano walichukuliwa.

Hii ni mara ya pili katika kipindi cha wiki tatu sasa.

Mwanzo wa muhula huu mwaka huu majambazi tena walivamia shule hiyo wakati wa usiku na kuwaiba mbuzi 27.

Wanafunzi shuleni humo wameiambia Radio Jangwani kuwa kumekuwa na visa vya wizi shuleni humo vinavyotekelezwa na watu kutoka nje. Wamesema kwamba waliporudi shuleni baada ya likizo iliyolazimishwa na virusi vya corona walipata baadhi ya vitu vyao vikiwa vimeibwa. Wanasema hata masanduku yao yalikuwa yamevunjwa na washukiwa wa wizi.

Hata hivyo shughuli za masomo zinaendelea kama kawa. Mwalimu mkuu amesema bodi ya usimamizi wa shule hiyo itakutana wiki ijayo siku ya Ijumaa ili kujadili swala hilo.

 

 

Subscribe to eNewsletter