Local Bulletins

Hofu ya makali ya virusi vya Ukimwi Marsabit

 

Na Isaac Waihenya

Watoto 11 kati ya 100 wanaozaliwa hapa jimboni Marsabit wapo katika hatari ya kuambukizwa virusi vya ukimwi.

Kwa mujibu wa mratibu katika idara inayoshughulikia watu wanaoishi na virusi vya HIV katika kaunti ya Marsabit Wario Arballe, ni kuwa kiwango cha maambukizi kutoka kwa mama hadi kwa mtoto kipo katika asilimia 11 kwa sasa.

Akizungumza na waandishi wa habari Wario amesema kuwa kwa sasa watu 2,887 wameambukizwa virusi hivyo ikiwa ni asilimia 1.2 ya maambukizi.

Amewataka wananchi kusita kuwatenga watu wanaoishi na virusi hivyo kwani wengi wao wanakumbwa na msongo wa mawazo kutokana na unyanyapaa.

Aidha Wario amesema visa vya mimba za mapema vimetajwa kuongezeka jimboni huku kati ya mwezi Oktoba na Disemba mwaka jana zaidi ya wasichana 200 wakipata ujauzito. Hii ni sawa na wasichana 66-69 waliotiwa mimba kila mwezi kati ya Oktoba na Desemba mwaka jana.

Wario ameyasema hayo wakti wa Mkutano wa hadhara uliowaleta pamoja maafisa wa afya jimboni, maafisa wa usalama, idara ya magereza sawa na waandishi wa habari ili kutafuta mustakabali wa jinsi ya kupunguza kiwango cha unyanyapaa jimboni ambacho ametaja kuwa kwa sasa kipo kati ya asilimia 40 hadi 45.

 

 

 

Subscribe to eNewsletter